Monday, June 2, 2014

KARIBUNI, DHANA NA FASILI(MAANA) YA LUGHA

Wapo wataalamu mbalimbali waliojaribu kuifafanua maana ya lugha kwa mfano Mgullu(1999) katika kitabu chake cha Mtalaa wa Isimu akirejelea mawazo na maoni ya wataalamu mbalimbali amejaribu kuifafanua maana ya lugha kama ifuatavyo.


Trudgil,(1974)anasema "Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zinazotumiwa kwa mawasiliano miongoni mwa watu wa jamii fulani yenye utamaduni wake"

Sapir,(1921) anasema "Lugha ni mfumo ambao mwanadamu hujifunza ili autumie kuwasilishia mawazo, maoni na mahitaji. Mfumo huu hutumia ishara ambazo hutolewa kwa hiari"

Weber,(1985) anasema "Lugha ni mfumo wa mawasiliano ya mwanadamu ambao hutumia mpangilio maalumu wa sauti kuunda vipashio vikubwa zaidi kwa mfano mofimu, maneno na sentensi" Pia anadai kuwa lugha ni mfumo wowote wa mawasiliano ya watu kwa mfano lugha ya Kifaransa. lugha ya Kihindi.

Kamusi ya TUKI(1990)inasema,"Lugha ni mfumo wa sauti zinazotumiwa na watu wa jamii fulani wenye utamaduni unaofanana ili kuwasiliana"

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa lugha ni mfumo wa sauti za nasibu ambazo zimekubaliwa na jamii ya watu fulani ili zitumike katika kukidhi mawasiliano yao ya kila siku katika nyanja mbalimbali za maisha mfano siasa, uchumi na utamaduni. Kutokana na maana mbalimbali za wataalamu hao walionukuliwa na Mgullu(1999) tunapata mambo ya fuatayo yanayounda au yanayopatikana katika lugha yoyote ile kama;

a) lugha ni mfumo wa sauti. Sauti mbalimbali zinazopatikana katika lugha fulani hupangwa kwa namna ambayo sauti hizo huungana pale zinapotamkwa (au kuandikwa) kutoka sehemu mbalimbali katika mfumo wa utamkaji (utazungumziwa katika mada zijazo)

b) lugha ni sauti za mawasiliano: lengo kuu la lugha yoyote ni kukidhi mahitaji ya mwanadamu ambayo ni mawasiliano. Mawasiliano hayo husaidia katika kupanga,kuagiza na kutimiza mambo mbalimbali ya maisha ya kila siku ya mwanadamu.

c) lugha ni sauti za nasibu:Hakuna mwanadamu anayezaliwa akiwa anafahamu lugha bali hukutana nayo kibahati mbaya tu. Hujifunza tu pale anapowasiliana na watu au pale mtu anapozungumza na yeye kusikilza na kuiga mfano mtoto mdogo anapofikia umri wa kuanza kuongea hujifunza kutamka silabi au maneno macache taratibu mwishowe hutamka sentensi nzima. Vile vile dhana ya unasibu katika lugha ni kwamba hakuna mahusiano ya moja kwa moja kati ya kiashiria au kitaja(neno au jina) na kiashiriwa au kitajwa(kile kinachotajwa). Hakuna uhusiano kati ya neno meza na kitu chenyewe ambacho kinaitwa meza.

d) lugha ni sauti za nasibu za kusemwa na watu: binadamu ndiye kiumbe pekee mwenye kutumia lugha, wanyama ndege na viumbe wengine mfano wadudu wao hawana lugha hata kama wanatoa sauti mbalimbali zinazowawezeshs kuwasiliana. Kwa mfano Trudgil(1980) akinukuliwa na Mgullu(1999) anasema sauti za nasibu ambazo hutumika katika mawasiliano ni za wanadamu. Sauti hizi vilevile huweza kuwasilishwa kwa kutumia alama maalumu yaani maandishi ingaw pia chaweza kuwa kigezo dhaifu sana kubainisha unasibu wa lugha ya mwanadamu kwani alama hizo pia huashiria sauti za kusemwa na watu.

e) lugha kama chombo cha utamaduni fulani: kila lugha ina utamaduni wake. Lugha yoyote ile hutumikia utamaduni wa watu fulani hivyo basi hakuna lugha bora duniani kuliko lugha nyingine kwa mfano lugha ya Kiingereza si bora duniani kuliko Kichina , Kihispania, Kijerumani au Kiswahili hata kama Kiingereza kinatumika kila kona ya dunia hasa kwa shughuli za kimataifa ikiwa lugha hii ilisambazwa na Waingereza kipindi cha ukoloni sehemu mbalimbali duniani.

f) lugha ni njia ya mawasiliano: lugha yoyote ile lengo lake kuu ni kukidhi haja ya mawasiliano kati ya mtu na mtu au mtu na kundi au watu na watu. Hivyo kama lugha haikidhi mawasiliano haina maana.

FAIDA ZA LUGHA


Kulingana na maelezo hapo juu lugha ina faida nyingi kama ifuatavyo:
Chombo cha mawasiliano miongoni mwa watu

Chombo cha kukuza utamaduni wa jamii fulani kwani lugha yoyote lazima iwe na utamaduni wake kulingana na jamii ya watu husika mfano naman ya kutumia lugha kw akusalimiana
Inaunganisha watu, lugha huunganisha watu wa jamii na mataifa mbalimbali kupitia ukalimani na utafsiri
Kitambulisho
lugha pia huweza kuwa kama kitambulisho cha utaifa au kabila mfano Mtanzania anayezungumza Kiswahili akiwa ughaibuni nje ya nchi yake na kukutana na mtu kutoka Tanzania anayejua kiswahili atafamika mapema pindi atakapozungumza.
]Lugha ina uwezo wa kukuza fasihi ya jamii husika iwe kwa njia ya maandishi au mazungumzo.

HASARA ZA LUGHA.

 >Hasara kuu ya lugha ni utengano. Jamii huweza kutengana kwa kukosa mawasiliano pindi wakutanapo watu wasiofahamu lugh kila mmoja lugha ya mwenzake huwa kama bubu japo kwa muda mfupi.

MAREJELEO


Mgullu,R.S(1999)Mtalaa wa Isimu,Fonetiki,Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili, Nairobi Kenya, Longhorn Publishers(Ukurasa wa 6 hadi 10)


Chanzo cha habari hii: http://tanzaniaswahili.blogspot.com/2013/01/



No comments:

Post a Comment